Nimeketi kitandani, nikatazama picha hii, nikatabasamu.
Hakika ni sanaa iliyofana.
Kwanini picha hii? tena ambayo bado haijakamilika?
Hayumkini ni kwasababu imeakisi utu wangu, ya kwamba mimi si mkamilifu.
Natazama nilipotoka. Nashusha pumzi. Natabasamu. #UZI
#DaktariMwandishi
Kwa sababu fulani, machozi yananilenga.
Nafumba macho. Taa zimezimwa. Chumba kipo kimya. Wenzangu wawili wametoka, mmoja amelala, siku yake haikuwa njema.
Sauti ya pekee ni ya feni inayozunguka kutupunguzia joto la jiji hili.
Navuta hisia. Mawazo yanarudi nyuma. Kumbukumbu
za tangu nikiwa mdogo. Nikiwa nisiyejua ya dunia. Nakumbuka kisiwani Mafia, rafiki yangu mzungu Samantha, na mdogo wake, Christopher. Najiuliza, wako wapi? Nawakumbuka Dorothea, Geo, Mselo, Mlekwa na Waziri. Namkumbuka Mama Mchungaji, alikuwa mwalimu mkuu wangu chekechea, alikuwa
wa kwanza kuniamini. Na kunionyesha kuwa, wanawake wanaweza.
Naikumbuka siku tuliyoenda mnarani na Marehemu mamamdogo Stella, ilikuwa mara ya mwisho kumuona hai. Nayahisi machozi yakitiririka mashavuni mwangu. Namkumbuka sana.
Naikumbuka siku ile tuliyohama, tulipoiaga Mafia.
Giza limetanda machoni mwangu. Nimezama kwenye mawazo. Nakumbuka Lushoto, kama mkanda wa video, nakumbuka nikiwa na binamu yangu Mamy, tumebeba viroba vya majni ya ng'ombe, mifagio, vidumu na mabegi yetu tukielekea shuleni asubuhi. Baridi ikitupiga, tunakaza mwendo kuwahi namba.
Nawakumbuka Zuhura, Frank Yuda, Elieza(Mungu ailaze roho yale mahali pema peponi) na Abubakari. Hawa tulicheza nao sana harusi. Nanong'ona, "Eeh Mungu, walinde huko walipo."
Naikumbuka siku tuliyohama Lushoto. Nilivyolia kumuacha binamu yangu kipenzi, Mamy. Safari ya Namtumbo.
Nakumbuka siku mama aliyonichapa kwasababu nilienda kuangalia mpira hadi saa moja usiku. Shule yetu ilikuwa inacheza na shule ya Rwinga. Nilirudi sauti imekauka kwa kushangilia. Vumbi jekundu la Namtumbo limejaa hadi kichwani. Nacheka ninapokumbuka hasira za kuchapwa.
Namkumbuka rafiki yangu Mabaga, Kasimu Rehani, Mwajuma, Shufaa, Nasorro Kipa, Yasini, Zuberi, Rama Madevu, Issa Kiduchu, Jafari, Mabula, Maisha, Shamira na wengine wengi. Eeh Mola, walinde, watimizie haja za mioyo yao.
Nakumbuka siku tulizocheza rede, kipindi cha mfungo wa
Ramadhani. Na siku zile za kutisha. Nyakati ambazo wavulana walipewa jukumu la kutusindikiza kuhakikisha kila msichana amefika kwao, kwasababu kulikuwa na watu wanakata matiti na sehemu za siri za watoto wa kike. Akili inaganda kidogo, nawaza namna gani ule upepo ulipita ukapotea
Alhamdulillah, hilo liliisha.
Naikumbuka siku ya kwanza sekondari, nikiwa nimetoka shule ya serikali, kijijini. Namna nilivyokuwa nikiwashangaa wale wa St.Mary's. Nakumbuka nilivyoumwa. Pumu ya ngozi. Najihisi nimeketi kitandani kwangu, bweni la Bibi Titi, nikitazama vidonda
vyangu, nikikumbuka maneno ya mwenzangu aliyenikataza nisiguse kitu chake, nitamuambukiza. Nakumbuka nilivyokuwa nikijitenga na kuketi nje ya darasa. Nakumbuka siku nyingi nilizolia. Nilizomuuliza Mungu, kama kuna kitu nimemkosea akanipa ugonjwa huo. Nakumbuka nilivyojishuhudia
nikipoteza kujiamini. Nikiuchukia mwili wangu. Kila nilipoamka na kuona vidonda baada ya kujikuna usiku kucha. Siamini kama sasa, ni miaka imepita tangu kupatwa na attack ya pumu ya ngozi.
Machozi yanatiririka mashavuni mwangu. Ni machozi ya maumivu na furaha. Makovu ya kihisia
bado mabichi. Bado najifunza kujipenda upya. Kujiamini. Kuyakubali makovu yangu kama sehemu ya maisha yangu.
Namkumbuka rafiki yangu mpenzi, Liz-Mindy, tumekuwa marafiki miaka 11 sasa. Naye ameyapitia hayo ya pumu ya ngozi.
Nakumbuka nilipomwambia, "mbona yako ina afadhali?
mwenzio nipo kama chui"
Nafuta machozi mashavuni. Natabasamu. Macho yangali yamefumbwa.
Kumbukumbu zinanipeleka Mazinde. Siku za kusimamia usafi, kwa nguruwe, siku za kuandaa mahafali na siku zote nilizoshinda nikisubiri kwa hamu kuona basi la Shambalai ili nilishangilie.
Ni kama filamu, nipo Maramba. Churwa, shambani na ndoo yangu navuna mahindi. Napeleka, annaisimamisha CO Meja Ngairo, ananiambia nirudi kujaza ndoo mahindi. Naondoka, nazama shambani, sirudi. Nalala kusubiri filimbi ya chakula.
Nakumbuka usiku wa madoso na chenja. Walionishika
mkono kwenye mabio. Nawakumbuka maST wenzangu. MaMTM nilipokuwa nawaoshea vyombo na kuwapigia kiwi. Nakumbuka namna ule wimbo wa, "Zaina Zaina (Zaina), Zaina mtoto (Zaina), mtoto wa kidigo (Zaina), lete raha (Zaina)", ulivyokuwa unaisuuza roho yangu na kunipa morali kukimbia.
Naikumbuka siku ya kwanza Kairuki, nikimbembeleza Hostel meneja anipe chumba. Nakumbuka mama alivyonisindikiza hadi chumbani na kunitandikia kitanda. Tukakaa. Moyoni siamini kuwa ndio safari ya udaktari imeanza.
Nayasikia machozi ya furaha yakinilenga. Ni miaka minne iliyopita.
Nakumbuka siku ya kwanza wodini. Sikujua niongee nini na mgonjwa. Nakumbuka siku ya kwanza mtoto alipofariki. Nililia usiku kucha. Nakumbuka nikiwafuata nyuma interns wanifundishe. Nikiwasumbua hadi wanakubali niende nao. Nacheka. Natabasamu
Nashtuka, mkanda wa kumbukumbu umeisha
nipo wakati uliopo.
Nafikiria research, mitihani na mipango yangu ijayo.
Naifikiria biashara yangu changa.
Nawaza kama nitaendelea kuandika makala magazetini. Je, nitakuwa daktari mzuri? Lakini, yafaa nini kuhofu kuhusu yajayo?
Septemba 11, 2016 asubuhi nalikuwa nikiwaza matokeo
yangu ya mwaka wa kwanza. Jioni yake, nilikuwa nimelazwa Bochi, nikipigania maisha yangu baada ya kunywa dawa ambayo bahati mbaya ime-expire. Naikumbuka vema siku hii. Namna nilivyokosa pumzi. Nilivyolia sababu kifua hakikuweza kuingiza wala kutoa hewa. Nilionja kifo. SITASAHAU
Ya nini kuhofu kuhusu yajayo sasa? Mwenyezi Mungu afahamu hayo.
Nafumbua macho yangu na kuona namna safari ya maisha yangu imenipeleka mbali na kunifundisha mengi. Natabasamu. Hakika tunatoka mbali.
Tunavuka mabonde na milima.
Tunaanguka. Tunakata tamaa. Tunaumizwa. Tunajutia.
Tunafurahi. Tunajifunza. Tunasamehe. Tunabariki. Tunapenda. Tunapendwa. Tunalaani. Tunabeba vinyongo. Tunaendelea kutobu vidonda.
Yote ni maisha.
Kwenye chumba cha marehemu Babu yangu, Dr.Nasetsi alikuwa na kikaratasi kimeandikwa, "MAISHA NI NINI?"
Nilikuwa nimekariri yote lakini
kwasasa nakumbuka haya tu:
"Maisha ni SAFARI, JARIBU.
Maisha ni WAJIBU, TIMIZA.
Maisha ni FUMBO, FUMBUA.
Maisha ni ZAWADI, IFUMBATE.
Maisha ni MAPIGANO, PIGANA."

Tazama ulipotoka, yaelewe mazuri na mabaya, vicheko na vilio, hasira na furaha, maumivu na raha uliyopitia.
Yatumie hayo kusonga mbele.
Andaa mpango wa yajayo. Furahia wakati uliopo. Jenga yaliyopo mbele yako.
Kwasababu, hakika maisha ni FUMBO na maisha ni SAFARI.
Nimeandika mengi. Nikuage kwa maneno ya Samba Mpangala akisema, "Dunia tunapita, kila kitu kitabakia"
#DaktariMwandishi đź‘Ł
You can follow @Kudu_ze_Kudu.
Tip: mention @twtextapp on a Twitter thread with the keyword “unroll” to get a link to it.

Latest Threads Unrolled: